Na Regina Mpogolo.
JUZI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea mpaka wa Holili
uliopo Tanzania na Kenya
katika wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro
alisema mpaka huo hauko
salama kutokana na kuwapo kwa njia nyingi za
panya ambazo wahalifu
hutumia kupitisha silaha
na bidhaa za magendo.
Waziri Mkuu alisema
uwepo wa njia nyingi za
panya katika mpaka huo
inahatarisha usalama wa
nchi zote mbili, Kenya na
Tanzania na kwamba matukio ya uhalifu yanayoendelea kutokea katika baadhi
ya mikoa iliyopo mipakani
ni dalili mbaya kwamba
mipaka haipo salama.
Pamoja na kwamba Waziri Mkuu aliyataka majeshi
ya Kenya na Tanzania kwa
kushirikiana na idara za
uhamiaji kuanzisha mfumo
wa pamoja wa usalama ili
kuhakikisha kwamba hakuna
mtu anapita na kufanya
uhalifu, naamini kwamba
wananchi wana jukumu
kubwa la kuimarisha ulinzi
huo wakishirikiana na
majeshi hayo.
Watu ambao wanapita
katika mipaka hiyo iwe wanaingia hapa nchini au wanatoka kuingia Kenya, kuna
watu ambao wanajua mbinu
zao lakini wanakaa kimya na
kuona kuwa sio kazi yao, ni
kazi ya majeshi.
Majeshi yetu hayawezi
kuwepo kila mahali na kwa
wakati wote lakini wanakopita wahalifu hawa iwe ni
kwa kupitisha bidhaa zao
kwa namna yoyote ile kuna
watu ambao huwaona au
wanashirikiana nao ambapo
wakitoa ushirikiano itasaidia
sana.
Majeshi haya yanahitaji
ushirikiano mkubwa kutoka
kwa wananchi ili waweze
kutokomeza uhalifu ambao
unafanyika mipakani au
magendo ambayo yanapitia
njia za panya katika mipaka
yetu.
Tukitambua kwamba
ulinzi wa nchi ni jukumu
letu sote hatutakaa kimya,
hata kama ni kwa kutoa taarifa tu kwa mamlaka husika
itasaidia kwa kiasi kikubwa
kubaini mbinu zao na pia
kuwakama.
Kuna biashara ambazo
pia zinapita katika njia hizi
za panya, tukumbuke kwamba bidhaa hizo ndizo ambazo
zinaingizwa sokoni bila
kulipiwa ushuru wala kodi
zozote na kuuzwa kwa bei
chini kuliko ile ya kawaida
huku nyingine zikiwa katika
ubora hafifu au zisizofaa
kabisa kwa matumizi.
Lakini zikiingia sokoni zinakutana na bidhaa ambazo
zimepita njia sahihi, kukaguliwa ubora wake na kuthibitishwa na pia kulipiwa kodi
mbalimbali.
Bidhaa hizi mbili zikikutana sokoni wote tunajua
nini kinachotokea, watu
watakimbilia kununua zile
zenye bei nafuu na kuhatarisha afya zao na maisha yao
na kuziacha zile zenye ubora.
Aidha, kwa kuruhusu
kuingiza bidhaa hizi kwa
njia za panya inachangia kwa
kiasi kikubwa kuua soko la
bidhaa za ndani ambazo kiuhalisia zinakuwa na ubora
mkubwa.
Kuna wananchi ambao
wanaishi mipakani lakini hawana uzalendo na nchi yao,
wao ndio ambao wanakuwa
vinara wa kuwapokea
wahalifu na wengine kuficha
silaha au bidhaa zao za
magendo katika nyumba zao
lakini hawatoi taarifa popote.
Ulinzi wa taifa letu uko
mikononi mwa kila mmoja
wetu kwa kuhakikisha
anakuwa mlinzi popote
alipo, kuhakikisha kwamba
hakuna mbinu chafu itapangwa mbele yake na akakaa kimya bila kuripoti na
pia hakuna bidhaa au silaha
zitapitishwa kimagendo.
Kwa upande wa majeshi
yetu ombi kwao watoe
ushirikiano mkubwa kwa
wananchi wema ambao
watajitolea kutoa taarifa za
uhalifu wa aina hii, wawe
wepesi kupokea taarifa na
kuzifanyia kazi mara moja na
kwa usiri mkubwa.
Itavunja moyo kama
mtu atajitolea kutoa taarifa ya mbinu za uhalifu au
ameshuhudia tukio fulani
lakini kukawa na uzito wa
kufanyia kazi au isifanyiwe
kazi kabisa na uhalifu ule
ukaendelea na kuathiri watu.