_______________
Na, Francis Daudi
Saa sita kamili usiku wa Desemba 9, 1961 Mwenge wa Uhuru uliwashwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Brigedia Alex Nyirenda, tukio hilo lilikwenda sambamba na kupandishwa kwa bendera ya uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa Taifa wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Kwa ujasiri mkubwa Brigedia Nyirenda alitekeleza maagizo ya Mwalimu Nyerere kupandisha Bendera ya Taifa na Mwenge wa Uhuru kwenye kilele kirefu kuliko vyote Afrika. Ilikuwa ni safari yenye hatari kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na barafu nyingi pamoja na mashimo na watu wengi waliogopa wakiamini kuwa uwezekano wa kurudi chini ukiwa hai ulikuwa mdogo sana.
Nyirenda aliongoza msafara wa watu 11 kwenye safari ya siku 16 kutoka Dar es salaam mpaka kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro. Ilikuwa safari ya kizalendo iliyohitaji kujitoa. Waliporudi Dar es salaam ilikuwa furaha mno na walipokelewa na Rais Nyerere ambaye alikuwa pamoja na mume wa Malkia wa Uingereza (Duke of Edinburgh) aliyefika kuhudhuria sherehe za uhuru. Hivyo basi Brigedia Alex Nyirenda ni sehemu muhimu ya historia tunapoadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Taifa Letu!
Alex Gwege Nyirenda alizaliwa tarehe 2 Februari 1936 eneo la Karonge, nchini Malawi. Mama yake alikwenda kumtembelea ndugu yake huko akiwa mjamzito na kubarikiwa kupata mtoto ingawa familia ya Nyirenda ilikuwa hapa Tanganyika. Alijiunga na shule ya msingi Mchikichini, Dar Es Salaam kisha Shule ya Sekondari ya Wavulana Malangali, Iringa( Pia mimi Francis Daudi, Nilisoma katika shule hii. Wengineo waliopata kusoma hapo ni Jaji Mkuu wa zamani Francis Nyalali, Kocha Mziray, David Mwaisela, Mark Mwandosya, Joseph Mungai, Adam Sapi Mkwawa, MaDC kama John Mwaipopo(Igunga) na Festo Kiswaga(Bariadi)
Nyirenda alichaguliwa Mkuu wa Bweni na baadaye Kiranja Mkuu shule ya sekondari Malangali, Kisha alijiunga Shule ya Tabora Boys hapo alisoma na Brigedia Mstaafu Hashimu Mbita na Bakari Mwapachu (kaka wa Juma Mwapachu). Alichaguliwa kujiunga Chuo cha Kifalme cha Kijeshi cha Sandhurst akiwa na aliyekuja kuwa Mkuu wa JWTZ Mrisho Sarakikya na S.M Kashmir ambaye alikuwa na asili ya Asia. Sarakikya aliondolewa kwa zengwe kuwa alianguka mtiani wa kiingereza. Nyirenda alikuwa kwenye kombania iliyoitwa Waterloo mwaka 1957. Baada ya mafunzo alirudi Tanganyika na kujiunga na King’s African Rifles(KAR) mwaka 1960.
Mwaka 1961 alipewa jukumu na Baba wa Taifa, Mwalimu JK Nyerere la kupandisha bendera ya Taifa letu kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, Nyerere alisema, ‘Sisi tunataka kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, Umulike hata nje ya mipaka yetu. Ulete tumaini pale ambapo hakuna tumaini, Upendo palipo na chuki na heshima palipojaa dharau’. Nyirenda aliongoza msafara wa watu 11 kwenye safari ya siku 16 kutoka Dar es salaam. Alipanda kwenye kilele cha Mlima(Kwa sasa kinaitwa Uhuru Peak) majira ya Saa5 usiku na kuuwasha mwenge wa uhuru, kisha kusimika bendera ya taifa usiku wa Desemba 9, 1961.
Alipanda uBrigedia siku moja, yeye na Brigedia Moses Nnauye(Baba mzazi wa Mbunge wa Jimbo la Mtama, Mh. Nape Nnauye). Kwenye kitabu Tanganyika Rifles Mutiny January 1964 kinataja ushiriki wa Nyirenda kwenye jaribio la Kuipindua serikali mwaka 1964. Kinaonesha Nyirenda kama mtu aliyetarajiwa kuwa mkuu wa jeshi hasa kutokana na uwezo wake kiuongozi na ukaribu na wanajeshi Waingereza.
Kutokana na tuhuma nyingi, Brigedia Nyirenda alijitoa jeshini mwaka 1964. Hadi umauti unamkuta anaeleza yeye alifungwa kwenye kambi ya Calito(Lugalo ya sasa) Hivyo hakuwa sehemu ya uhasi ule. Shutuma zingine zilikuwa kwamba yeye ni Mmalawi. Alikubali kuzaliwa Malawi lakini uzalendo wa Nyirenda hukupaswa kutilia shaka hasa kwa kazi zake. Brigedia Alex Gwege Nyirenda alifariki Jumapili Desemba 21, 2008 kutokana na saratani ya koo. Jina la Nyirenda lina nafasi muhimu katika historia tunapoadhimisha miaka 57 ya Taifa letu.
Nimeielezea historia Brigedia Alex Gwege Nyirenda kwani kuna watu husema, alifariki baada ya kuufikisha mwenge kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Ieleweke, hata vita vya Kagera, Nyirenda hakuwa jeshini. Kwa wakati huo alikuwa Zambia akifanya kazi kwenye kampuni binafsi.
Niwatakie heri katika sikukuu hii muhimu, Hatuna Tanzania ingine tofauti na hii. Wao wanapaita ‘Tanzania’ sisi tunapaita ‘Nyumbani’. Tuitunze nchi hii kwa vizazi vijavyo!
Imeandaliwa Na Francis Daudi.
Idumu Daima Tanzania
Udumu Daima Uhuru