Kiwanda cha matairi cha General Tyre kiliuawa na ufufuaji wake unahujumiwa! - Yajayo Yanafurahisha | "Muda Unaongea"

Yajayo Yanafurahisha | "Muda Unaongea"

"Muda Unaongea"

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

23 Feb 2019

Kiwanda cha matairi cha General Tyre kiliuawa na ufufuaji wake unahujumiwa!

Kiwanda cha General Tyre ni moja ya viwanda bora kabisa kuwahi kutokea EAC na Afrika ya kati. Kiwanda hicho kimekuwa kikiendeshwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania ambayo nadhani ina hisa asilimia 76 na kampuni ya Continental ya Ujerumani ambayo ina hisa asilimia 24.
Related image
Soko kubwa la kiwanda hicho lilikuwa ni Afrika mashariki na kati. Nilipotembelea kiwandani hapo mwaka 2008 na kuzungumza kwa kirefu na Meneja wa Kiwanda (Factory Manager) ndugu Mnzava, tulielezwa kwamba kiwanda kilikuwa hakijafikia uzalishaji wa kutosheleza soko la Afrika mashariki na kati.
Kiwanda hicho wakati kikifanya kazi kilikuwa na ofisi zake kuu hapo hapo Njiro jijini Arusha, kilikuwa na depot nchini Kenya, Malawi na Uganda. Kilikuwa kinaajiri wafanyakazi wapatao 529 pale ofisi kuu bila kuhesabu waliokuwa kwenye depot zake kwenye hizo nchi tatu za Afrika mashariki na kati. Kama kuna maajabu basi ni haya. Kwamba unafanya biashara, una wateja wanaokuzidi uwezo, yaani kila unachozalisha kinachukuliwa na hakitoshi, lakini biashara yako inafilisika! Hayo yanatokea hapa Tanzania.
Lakini nini hasa sababu ya kufa kiwanda hiki? Wafanyakazi wanasema ni lazima serikali iunde kamati ndogo ya kuchunguza chanzo hasa cha kufa kwa kiwanda cha general tyre. Ili kwamba kabla ya kuondoa mahindi mabovu, tujue chanzo cha wadudu wanaotoboa mahindi. Kwamba huwezi leo kufufua kiwanda wakati waliokiua bado wako mle mle. Kwa mfano, wafanyakazi niliozungumza nao wameelekeza lawama zao kwa uongozi wa kiwanda kwamba uchunguzwe kwa kuwa wanaona ndiyo sababu hasa ya kufa kwa kiwanda kupitia ufisadi. Wangependa aliyekuwa Afisa mwajiri na meneja rasilimali watu wahojiwe pamoja na mameneja wote waliokuwepo. Wanahisi hawa wanajua vizuri kilichotokea.
Lakini pia wafanyakazi hao wametaka serikali ichunguze na kujua kama kuna watanzania wana hisa kwenye kampuni ya matairi ya YANA ya Kenya, au kama kuna watanzania walikuwa na mahusiano na kampuni hiyo ya Kenya. Kwa kuwa wao wanaamini kabisa kwamba kuna mchango wa watanzania wenzetu kuua general tyre ili YANA iuze matairi yake hapa kisha wao wapate mgawo wao kutoka YANA. Wanataka pia meneja wa kiwanda ahojiwe kwa nini mpira wa Kenya ulikuwa unakuja kutwanga kwenye burmbary ya general tyre kwa kuwa wanasema ulipoanza kutwanga huo mpira hapo, burmbary ile ikaanza kuharibika kila mara.
Wafanyakazi hao wanasema Continental haihusiki na kufa kwa kiwanda, inasingiziwa. Kwa mfano menejimenti ilikuwa inadai kwamba continental walikuwa wanadai mgawo wao wa bilioni 3. Swali wanalojiuliza wafanyakazi hao ni kwamba, ilikuwaje continental isipate mgawo wake mpaka iidai serikali wakati meneja mkuu (General Manager) alikuwa anatoka Continental. Aliwezaje kupeleka mgawo wa serikali akaacha mgawo wa mbia aliyemweka pale?
Miongoni mwa sababu zinazofanya wafanyakazi wa General Tyre wadai kifo cha kiwanda kile kilisababishwa na menejimenti na mafisadi waliokuwa nje ya kiwanda ni kitendo cha menejimenti wakati fulani walidai computer imepotea yenye nyaraka zote za general tyre. Bila shaka huo ulikuwa ni mchezo wa pale pale ndani ya menejimenti. Kiwanda kile kilichokuwa na ulinzi na ambacho hakikuwahi kuvamiwa na majambazi, iweje computer ipotee ofisini kama haukuwa mchezo wa kuanza kukihujumu?
Lakini pia kuna wakati serikali ilitoa shilingi bilioni 12.6 kwa ajili kukifanyia kiwanda marekebisho makubwa ya kimfumo (restructuring). Kwa mshangao wao kama wafanyakazi kilichofanywa na menejimenti ya kiwanda ni ufisadi uliopitiliza. Kwanza menejimenti ilitengeneza masanamu mbele ya ofisi, kisha ikaanzisha timu ya mpira ya general tyre ambayo ilikuwa inatumia fedha nyingi sana. Lakini tatu wakakarabati ukuta wa kiwanda (fence) na kuuwekea madoido. Kwa waliofika Arusha wataona ukuta ule umepigwa rangi na sehemu zenye vyuma zimebandikwa matairi yalivyopigwa rangi katikati kupendezesha ukuta.
Lakini nne na balaa zaidi, kiwanda kilichimba kisima cha maji kwa shilingi bilioni 3. Mmoja wa wafanyakazi hao akaniambia hata juzi amepita eneo la Friends Corner jijini Arusha na kukuta mtaro unaochimbwa na mamlaka ya maji jijini Arusha (AUWSA) ingawa si mrefu sana lakini tayari wamefikia maji na kusababisha maji yajae mtaroni ambapo wanalazimika kuyatoa ndipo wafanye kazi. Sasa ilikuwaje general tyre wachimbe kisima kwa bilioni 3 ndipo wapate maji? Hicho kisima kina urefu gani kwenda chini?
Lakini pia wafanyakazi waliniambia kwenye mashamba ya general tyre yaliyolimwa kule Tanga, tayari mpira ulishapandwa. Lakini matokeo yake, mpra ule ukawa unatumika kuvuna utomvu na kupelekwa nchini Kenya kwenda kutengeneza chewing gum (Big G, Jojo, nk). Mpaka sasa hawajui mashamba yale bado ni ya General tyre au yameshauzwa! Kwa sababu wanasema ilifikia mahali mpaka eneo la kiwanda pale Njiro walitaka kuuza. Wafanyakazi hao wanasema walishtukia tu beacon zinasimikwa kwenye eneo la kiwanda na walipopiga kelele ndipo zikang’olewa.
Baada ya mkakati wa kukiua kile kiwanda kukamilika, wafanyakazi walishtukia tu wamepumzishwa nyumbani kiwanda kimefungwa lakini wakawa wanaendelea kulipwa mishahara kwa miezi kadhaa. Hapo ndipo wakaamua kujitokeza kwenye kituo kimoja cha televisheni na kuhoji inakuwaje wanalipwa mishahara halafu hawafanyi kazi? Wakasema je, siku hizo hela zinazowalipa mshahara zikiisha na hawazalishi nyingine, itakuwaje?
Ni baada ya kuonekana kimbelembele kuhoji wakati wanalipwa bila kazi, ndipo waliitwa kazini na mnamo Agosti 31, 2009 wakapewa barua ya kwanza ya kuachishwa kazi kwa kupunguzwa (retrenchment). Wakaanza kufuatilia nini kinaendelea mpaka wafanyakazi wanapunguzwa (retrenched) wote, nani anabaki ili kiwanda kiendelee? Mwezi mmoja tu baadaye yaani Septemba mwaka huo huo wa 2009, wakapewa barua ya pili ambayo sasa hiyo ilikuwa inasema wameachishwa kazi kwa ajili ya marekebisho ya mfumo (termination due to restructuring). Hapa wakadhani kwamba sasa wanapumzishwa kwa muda kisha baada ya marekebisho watarudi.
Wafanyakazi hawa wanashangazwa na maneno ya mbunge wao Godbless Lema bungeni kwamba kiwanda kihamishwe atafutwe mwekezaji mpya. Wanasema mnamo Januari 2011 walifika ofisi ya mbunge na kumweleza shida zao. Akawaahidi kufuatilia suala lao. Waliporudi mara ya pili akawaambiwa kwamba amefuatilia na amegundua hata cheque walizopewa zilikuwa feki. Kwamba malipo waliyopewa si kile walichostahili.
Lakini waliporudi kwake tena mara ya tatu akasema walicholipwa ni sawa na wamelipwa kwa mujibu wa sheria. 
Hapo wakaanza kujenga mashaka kwamba mbunge amepewa tayari kitu kidogo na mafisadi wanaotaka kiwanda hicho kife na wafanyakazi wapotelee mbali. Kilichowashtua zaidi ni pale alipoacha maagizo kwa sekretari wake kwamba wakija watu wa general tyre awaambie mbunge hayupo wakati yupo ofisini.

Wafanyakazi hao wanasema kauli ya mbunge wao Godbless Lema bungeni hivi karibuni kwamba kiwanda kihamishwe pale kilipo ina lengo la yeye kujipatia maslahi binafsi kifisadi na si kukisaidia kiwanda kufufuka. Wanasema waliwahi kusoma kwenye gazeti moja kwamba Lema akishirikiana na madiwani wa jiji la Arusha ambao wengi ni wa CHADEMA, walipendekeza kwamba kiwanda kile wapewe kampuni ya Simon Group wakifanye godown halafu kiwanda chenyewe kitajengwa Kisongo. Ni haya haya aliyoyafanya kwenye kamati ndogo ya bunge ya kamati ya hesabu za mashirika ya umma na ndiyo aliyoyarudia juzi akiwa bungeni akichangia taarifa ya kamati ya viwanda na biashara.
Ni dhahiri mbunge Lema ni miongoni mwa watu wanaohujumu kiwanda cha general tyre kisifufuliwe. Mapendekezo yake ni kuhakikisha kinaondoka pale ili watu wanaolitaka lile eneo walichukue na kumlipa yeye chake mapema kabisa. Ni sahihi kusema kwamba Kiwanda cha matairi cha General Tyre kiliuawa na ufufuaji wake unahujumiwa! Na mmoja wa watu wanaohujumu ufufuaji wa kiwanda kile ni mbunge mwenyewe wa jimbo la Arusha mjini ambaye alitakiwa kulia bungeni na ofisini kwa waziri wa viwanda kila siku mpaka kiwanda kile kifufuliwe. Godbless Lema mbunge ni mwakilishi wa wananchi au mfilisi wa wananchi?
Wafanyakazi wale wanasema wana ujumbe kwa mheshimiwa Rais Magufuli. Wanasema wanasema, “Tuna imani kubwa na Rais Magufuli. Amerudisha heshima ya taifa. Sasa hivi hata nikienda taifa lolote najivunia kusema mimi natoka Tanzania. Nchi ilikuwa imewekwa mifukoni mwa watu wachahe na kumilikiwa na familia chache. Sasa tunamwomba kwanza aunde timu ya watu wachache waadilifu wachunguze nini kilitokea. Kisha akifufue kiwanda hiki”.

Credit: Samson Mwigamba

Post Bottom Ad