Ahadi za JPM kutekelezwa 90% ifikapo 2020, Kassim Majaliwa - Yajayo Yanafurahisha | "Muda Unaongea"

Yajayo Yanafurahisha | "Muda Unaongea"

"Muda Unaongea"

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

25 Feb 2019

Ahadi za JPM kutekelezwa 90% ifikapo 2020, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifi kapo mwaka 2020. 

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii kama maji, afya, nishati, elimu na miundombinu zinapatikana kwa uhakika. Alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kituo cha Polisi cha Tarakea wilayani Rombo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro. Waziri Mkuu alisema wananchi waendelee kuwa na serikali yao ambayo imejipanga kutekeleza ahadi zote zilizotolewa na Rais Magufuli kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza. 

Pia, Waziri Mkuu alisema mtumishi mzembe, mwizi, mla rushwa na asiyewajibika hana nafasi katika serikali ya awamu ya tano, hivyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wote waimarishe utendaji wao. Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini. “Iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

” Waziri Mkuu alisema kwa sasa serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao. Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa kushirikiana na Madiwani wahakikishe wanaboresha masoko katika mipaka ya Holili na Tarakea ili yawe katika viwango vya kimataifa. Waziri Mkuu alisema iwapo masoko hayo yaliyo katika mpaka wa Tanzania na Kenya yataboreshwa yatawavutia na wananchi wa Kenya kuja kufanya biashara, hivyo kuiwezesha halmashauri hiyo kuongeza mapato.

Post Bottom Ad